Wandani wa Rais Ruto waendelea kujifariji baada ya UDA kushindwa Ol Kalou

Na Emmanuel Oyasi,
Mwakilishi wa kike wa kaunti ya Pokot Magharibi, Rael Kasiwai, amesema kushindwa kwa chama cha UDA katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou hakupaswi kutafsiriwa kuwa serikali ya Kenya Kwanza imepoteza uungwaji mkono wa wananchi.


Akizungumza katika hafla ya inua mama, wezesha jamii iliyoandaliwa na mwakilishi wa kike kaunti ya Kericho, Beatrice chepng’eno kemei, Kasiwai alisema matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa tukio la kipekee na hayawezi kutumika kupima mwelekeo wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Kwa mujibu wake, serikali ya Kenya Kwanza imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa usawa katika maeneo mbalimbali nchini, hatua ambayo imeendelea kuimarisha uungwaji mkono kwa rais William Ruto.


Alieleza kuwa kutokana na utekelezaji wa miradi hiyo, ana imani rais ruto atapata fursa ya kuhudumu kwa mihula miwili ya uongozi.


“Tumeona maendeleo mengi ambayo rais Ruto amefanya katika taifa hili. Na ndio maana tunasema aendelee kuongoza Kenya. Kuna wengine wanaongea tu eti wanataka rais Ruto aondoke na hawana sababu. Eti kwa sababu wametushinda tu katika uchaguzi mmoja sasa wanafikiria wameweza,” alisema Kasiwai.


Kwa upande wake mwakilishi wa kike kaunti ya Turkana, Cecilia Asinyen, alimkosoa kinara wa chama cha DCP, Rigathi Gachagua, kwa kile alichosema ni kushindwa kumpongeza na kumshukuru mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC), Erastus Ethekon, baada ya kufanikisha uchaguzi mdogo wa Ol Kalou.


Aidha asinyen alimtaka Gachagua kuheshimu taasisi huru za kikatiba na kuepuka matamshi ambayo, kwa maoni yake, yanaweza kupunguza imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi na taasisi za kidemokrasia.


“Juzi Gachagua alisema kwamba rais amemnunulia mwenyekiti wa IEBC nyumba eti ndio kura iibiwe, lakini tangu washinde uchaguzi wa Ol Kalou, nimesubiri sana kumwon Gachagua akimshukuru Ethekon kwa kusimamia uchaguzi huru,” aslisema Asinyen.