Wamiliki wa silaha kinyume cha sheria Pokot na Turkana wapewa makataa ya siku 7 kuzisalimisha

Na Benson Aswani,
Kamishina wa kaunti ya Pokot magharibi Khalif Abdulahi amewataka wakazi ambao wanamiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha katika kipindi cha siku saba zijazo.


Akizungumza baada ya kikao cha usalama kilichowaleta pamoja wadau wa usalama kutoka kaunti za Pokot maghaibi na Turkana eneo la Kainuk, Khalif alisema huenda oparesheni ya kutwaa silaha hizo kwa nguvu ikaendeshwa iwapo wahusika hawatatii agizo hilo.

“Tumekubaliana kwamba ndani ya siku saba, watu ambao wanamiliki silaha kinyume cha sheria wazisalimishe. Na wale ambao watakataa basi itatulazimu kutumia nguvu, si tu kuzitwaa bali kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema Khalif.


Aidha Khalif alitoa onyo kali kwa wanasiasa ambao wanafadhili makundi ya wahalifu katika kaunti hizo mbili akisema kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, akiwahimiza kutumia raslimali walizo nazo kuimarisha maisha ya wakazi.


“Nataka kuchukua fursa hii kuwaonya wanasiasa na wale ambao wanafadhili wahalifu kuharibu amani. Tunaenda kukabiliana nao ipasavyo. Badala ya kununua silaha kwa ajili ya watu wetu, wanapasa kufadhili elimu kwa watoto wetu,” alisema.


Kwa upande wake kamishina wa kaunti ya Turkana Julius Kavita alisema wametumia pia kikao hicho kujadili jinsi wakazi kutoka kaunti zote mbili watatumia kwa pamoja raslimali ambazo zinapatikana maeneo hayo ya mipakani bila ya mizozo.


“Kuna raslimali nyingi eneo hili na tumeelewana kwamba jamii zote mbili zinapasa kutumia raslimali hizi kwa usawa hasa madini, na tunataka serikali za kaunti hizi mbili kudhibiti shughuli hii ili uchimbaji madini utekelezwe tu na watu wetu hapa,” alisema Kavita.


Baadhi ya machifu waliohudhuria kikao hicho kutoka pande zote mbili pia walielezea mikakati ambayo wanaweka kuhakikisha kwamba hali ya usalama inaendelea kuimarishwa, huku pia wakipendekeza hatua ambazo zitasaidia kukabiliana na utovu wa usalama.