Wakulima watakiwa kununua dawa za mimea kutoka kwenye maduka yaliyoidhinishwa

Na Benson Aswani,
Wakulima katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kuwa makini wanaponunua dawa za mimea na kuhakikisha kwamba wananunua kutoka kwenye maduka ambayo yameidhinishwa na bodi ya bidhaa za kudhibiti wadudu, Pests Control Products Board (PCPB).
Akizungumza mjini Kapenguria baada kikao na wauzaji wa bidhaa hizo, meneja wa bodi hiyo eneo la kaskazini mwa bonde la ufa Anthony Wechuli aidha aliwataka wakulima kuhakikisha kwamba wanasoma maelezo kuhusu matumizi ya dawa hizo kabla ya kuzitumia ili kuzuia madhara ambayo huenda yakashuhudiwa.
“Nawahimiza wakulima kwamba wanaponunua dawa kutoka kwa maduka ya dawa, wahakikishe kwamba wananunua kutoka kwenye maduka ambayo yameidhinishwa, na pia kuhakikisha kwamba wanafuata maelezo wanapotumia dawa hizo kwa mimea,” alisema Wechuli.
Aidha Wechuli aliwataka wakulima ambao huenda hawana uhakika kuhusu jinsi ya kuweka dawa kwenye mimea yao kutafuta huduma kutoka kwa watu ambao wamepewa mafunzo kuhusu shughuli hiyo anaosema wanapatikana kote nchini.
“Iwapo mkulima hana uhakika na jinsi ya kuweka dawa kwenye mimea, ni vyema kwake kutafuta maafisa ambao wamepewa mafunzo maalum kuhusu jinsi ya kutekeleza shughuli hiyo. Maafisa hawa wanapatika kote nchini,” alisema.
Wakati uo huo Wechuli alitoa onyo kwa wauzaji wa bidhaa hizo dhidi ya kuwauzia wakulima bidhaa ambazo muda wake wa matumizi umepita, akiwataka kuhakikisha kwamba bidhaa wanazoweka kwenye maduka yao zinauzwa ndani ya muda uliowekwa.
“Baadhi ya watu wanaouza bidhaa hizi huwauzia wakulima bidhaa ambazo muda wake wa matumizi umekamilika. Natoa onyo kwa wauzaji kama hawa kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi yao wakipatikana,” alisema.