Wakulima wa maziwa wanufaika na mitambo ya kuhifadhi maziwa Pokot magharibi

Na Emmanuel Oyasi,
Ni afueni kwa makundi ya wakulima wa maziwa katika kaunti ya pokot magharibi baada ya serikali kuu kupitia wizara ya kilimo kusambaza mitambo mitatu ya kuhifadhia maziwa.


Mitambo hiyo inatarajiwa kusaidia kupunguza hasara inayotokana na maziwa kuharibika baada ya kuvunwa, na kuwapa wakulima fursa ya kuyahifadhi kwa muda mrefu kabla ya kuyapeleka sokoni.


Akizungumza wakati wa ugavi wa mitambo hiyo katika eneo la kabichbich, eneo bunge la pokot kusini, mkewe rais Bi. Rachel Ruto, alisema serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo na mifugo ili kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kuinua viwango vyao vya maisha.


Aidha, Bi. Rachael aliwahimiza wanachama wa makundi yaliyopokea mitambo hiyo kuitunza na kuitumia kwa njia inayofaa ili iweze kuwahudumia wakulima kwa muda mrefu na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.

“Mitambo hii itanufaisha zaidi ya nyumba alfu 3 kwa kupunguza hasara, kuhifadhi ubora wa maziwa na kuwasaidia wakulima kupata mapato zaidi kutoka kwa juhudi zao. Natoa wito kwa makundi ambayo yamepokea mitambo hii kuitunza vyema ili iwe ya manufaa kwao,” alisema Bi. Rachael.


Wakati uo huo, Bi. Rachael amesema kaunti hiyo ni miongoni mwa zile zenye rasilimali nyingi za maendeleo pamoja na viongozi wenye maono ambao wanaendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.


“Pokot magharibi ina kitu ambacho ni chenye thamani sana. Si tu mifugo wala ardhi, bali watu ambao wana juhudi kuu sana. Na ndio maana tunashirikiana na viongozi katika kaunti hii ili kuboresha maisha ya wakazi,” alisema.