Wakazi wa Turkwel kunufaika na huduma za kampuni ya KenGen

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amefanya kikao na meneja wa kampuni ya kuzalisha umeme ya KenGen, mhandisi Peter Njenga kuangazia utendakazi wa kampuni hiyo na jinsi itakavyowanufaisha wakazi wa maeneo ya Turkwel ambako kunazalishwa umeme.


Akizungumza na wanahabari baada ya kikao hicho cha alhamisi, gavana Kachapin alisema wamekubaliana na kampuni hiyo kuhakikisha kwamba wakazi hao wananufaika na maji safi ya matumizi, umeme katika nyumba zao pamoja na nafasi za ajira kwenye kampuni hiyo.


“Kuna huduma ambazo tunaona KenGen inaweza kutekeleza kwa ajili ya wakazi wa eneo la Turkwel, kama vile maji safi ya matumizi, umeme katika nyumba zao, ajira na ujenzi wa miundo msingi, na tumeelewana kwamba kampuni hiyo itaangazia maswala hayo,” alisema gavana Kachapin.


Aidha gavana Kachapin alisema wamekubaliana na uongozi wa kampuni hiyo kuhusu kurejeshwa eneo la Turkwel afisi zake ambazo zilihamishiwa mjini Kitale kaunti ya Trans nzoia kufuatia utovu wa uslama, hasa baada ya kuimarishwa hali hiyo.


“Tumezungumzia pia mambo ya afisi ya kampuni hiyo ambayo ilihamishiwa mjini Kitale kwa sababu ya usalama, na nimefurahi kwamba meneja amesema watarejesha kampuni hiyo Turkwel baada ya usalama kuimarishwa,” alisema.


Kwa upande wake meneja wa kampuni hiyo mhandisi Peter njenga alitoa hakikisho kwamba wataendelea kushirikiana na serikai ya kaunti hiyo kuhakikisha wakazi wa maeneo hayo wananufaika na huduma zake.


“Tuliona ni vyema tupitie katika afisi ya gavana tumsikilize na tuone jinsi ambavyo tutashirikiana kuhakikisha kwamba raslimali ambazo zinapatikana eneo hilo zinawanufaisha wakazi,” alisema Njenga.