Wakazi wa kambi karayi waonywa dhidi ya kukaribia machimbo ya dhahabu yaliyotelekezwa

Na Emmanuel Oyasi,
Wakazi eneo la Kambi Karayi na maeneo mengine ya kuchimba madini kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kutoendeleza shughuli ya uchumbaji madini katika machimbo ambayo yametelekezwa.
Akizungumza ijumaa siku moja tu baada ya wachimba migodi wanne kuaga dunia kwa kuporomokewa na mgodi eneo la Kambi Karayi, afisa wa idara ya madini kaunti hiyo Brian Bundi alisema maeneo haya ni hatari hasa wakati huu ambapo kunaendelea kushuhudiwa mvua.
Bundi alielezea kusikitishwa na vifo vilivyotokea mapema alhamisi kwenye machimbo hayo.
“Kama afisi tunatoa rambi rambi zetu kwa familia za waliopoteza wapendwa wao katika mkasa huu. Tunawaomba wakazi eneo hilo kutoendeleza shughuli ya kuchimba dhahabu kwenye machimbo ambayo yametelekezwa. Hii ni hatari sana hasa wakati huu ambapo tunaendelea kushuhudia mvua kubwa kaunti hii,” alisema Bundi.
Aidha alisema mikakati inaendelezwa ya kuhakikisha kwamba machimbo yaliyotelekezwa baada ya kusimamishwa shughuli ya uchimbaji madini kwa wachimba madini ambao walikuwa wakitumia mashine yanafunikwa.
“Tanaendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba maeneo hayo ya machimbo ambayo yalitelekezwa yanafunikwa ili kuzuia maafa zaidi. Tumeongea na watu ambao walikuwa wakifanya kazi maeneo hayo ili wayazibe,” alisema.