Wakazi wa Endough watakiwa kujisajili kupata vitambulisho vya kitaifa

Na Benson Aswani,
Mwakilishi wadi ya Endough kaunti ya Pokot magharibi Victor Siywat amepongeza idadi ya wakazi ambao wamejitokeza kuchukua vitambulisho katika zoezi ambalo limekuwa likiendelezwa eneo hilo.


Akizungumza na kituo hiki Siywat ambaye pia ni naibu spika wa bunge la kaunti hiyo alielezea umuhimu wa wakazi kuwa na stakabadhi hizo kwani kando na kutumika kupiga kura, zitawawezesha kunufaika na huduma muhimu kutoka kwa serikali.


Aidha Siywat aliwataka wale ambao hawajapata stakabadhi hizo na wametimu umri wa kuwa nazo kuwasiliana na afisi yake ili kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba wanazipata.


“Maafisa ambao wamekuwa wakisajili watu ili kupata vitambulisho wamekuwa eneo hili kwa ajili ya shughuli hiyo, na wakazi wamejitokeza kwa wingi kuchukua stakabadhi hiyo. Wale ambao labda hawakufikiwa na wametimu umri wa kupata vitambulisho, nawasihi wawasiliane na afisi yangu ili tuweke mikakati yao kupata,” alisema Siywat.


Wakati uo huo Siywat alitumia fursa hiyo kusifia hatua za maendeleo ambazo zimepigwa katika wadi hiyo katika kipindi ambacho amekuwa afisini, akiwahakikishia wakazi kwamba ataendelea kushirikiana na idara mbali mbali za serikali kuhakikisha wanapokea huduma bora.


“Nafurahi kwamba wadi yetu imepata maendeleo ambayo hatujawahi kuona wakati mwingine. Na nitaendelea kushirikiana na idara mbali mbali kuhakikisha kwamba tunapata huduma ambazo zinastahili,” alisema.