Wakazi Kacheliba wanufaika na huduma za matibabu kutoka wakfu wa Safaricom

Na Joseph Lochele,
Wakazi eneo bunge la Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi wamenufaika na matibabu ya bure katika kambi ya matibabu ambayo iliandaliwa jumapili kwenye shule ya upili ya wasichana ya Kacheliba, ambayo yalifadhiliwa na wakfu wa Safaricom.


Mbunge wa eneo hilo Titus Lotee aliwapongeza wakazi ambao walijitokeza katika kambi hiyo ya matibabu, ambapo magonjwa mbali mbali hasa yanayoaminika kuwa magonjwa sugu yaliweza kushughulikiwa huku pia walemavu wakipewa huduma mbali mbali.


Aidha Lotee alisema zaidi ya wakazi 20 eneo hilo wamesajiliwa katika bima ya afya ya jamii SHA na kulipiwa kwa mwaka mmoja na wakfu huo wa safaricom.


“Watu wamehudumiwa kwa njia tofauti. Wale ambao ni walemavu, wale ambao wana magonjwa sugu na wale ambao wana magonjwa ya kawaida wote wa meshughulikiwa. Ningependa kuwapongeza wakazi wa Kacheliba kwa kuja maana kama hawangekuja hatungekuwa na watu wa kuhudumia,” alisema Lotee.


Wakati uo huo Lotee alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakazi eneo bunge hilo kuendelea kujitokeza na kusajiliwa kwenye bima hiyo ili waendelea kunufaika na matibabu kwa gharama ya chini, akiwataka kuwapuuzilia mbali wanaokosoa utendakazi wa bima hiyo.


“Nawasihi watu wangu wa Kacheliba kujisajili kwa bima ya SHA ili wapate huduma za matibabu kwa gharama ya chini. Wasiwasikilize viongozi wa kisiasa ambao wanapinga bima hii, maana wao wenyewe wanaitumia,” alisema.