Wafanyikazi wa CICO Pokot Magharibi wagoma kulalamikia malipo duni

Na Benson Aswani,
Wafanyikazi wa kampuni ya kutengeneza barabara ya CICO wanaohudumu kwenye barabara ya Kitale-Lodwar eneo la Murpus kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia kunyanyaswa na kampuni hiyo wakidai kukiukwa haki zao.
Wakizungumza baada ya kuandaa maandamano, wafanyikazi hao wakiongozwa na Isaac Osundwa wanalalamikia miongoni mwa maswala mengine, mishahara duni ambayo walisema haitoshelezi mahitaji yao na familia zao hasa ikizingatiwa gharama ya juu ya maisha hapa nchini.
“Shida moja kubwa zaidi ni mshahara, kwa sababu tumekuja hapa kufanya kazi ili tufaidi jamii zetu, lakini sasa mshahara tunaopewa uko chini sana ikilinganishwa na gharama ya maisha hapa nchini,” alisema Osundwa.
Aidha wafanyikazi hao walidai kwamba uongozi wa kampuni hiyo umedinda kuwaruhusu kujiunga na vyama vya wafanyikazi ambavyo vitawasaidia kupigania haki zao, hali waliyosema inatumika kuwakandamiza.
“Tulikuwa tumejiunga na muungano wa wafanyikazi lakini sasa kampuni ilikuja na kutuambia kwamba tujiondoe kwenye muungano huo, hali tunafahamu kwamba haki zetu zitaweza tu kuheshimiwa tukiwa kwenye muungano,” alisema.
Waliapa kuendelea kususia kurejea kazini hadi pale matakwa yao yatakaposhughulikiwa, wakitoa wito kwa uongozi wa vyama vya wafanyikazi nchini kuingilia kati na kuhakikisha kwamba haki zao zinaheshimiwa.
“Iwapo kampuni haitaweza kushughulikia matakwa yetu, kama wafanyikazi tutasalia kwenye mgomo hadi siku ambayo haki zetu zitaweza kuzingatiwa,” alisema.
