Wadau walalamikia kutelekezwa shule za mashinani katika utekelezwaji mtaala wa CBE

Na Benson Aswani,
Wito umetolewa kwa serikali kuwekeza zaidi katika elimu ya watoto hasa maeneo ya mashinani ambako wanakabiliwa na changamoto za kupata huduma ya viwango vinavyostahili vya elimu ya CBE.
Wakizungumza katika shule ya msingi ya Kakpau, Chemwochoi eneo bunge la Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi, wadau wakiongozwa na mwanaharakati Naomy Kendagor walisema wanafunzi katika shule za maeneo ya mashinani wanakosa vifaa vya kufanikisha mtaala huo wa CBE.
Aidha Kendagor alielezea masikitiko kwamba shule zilizo maeneo ya mijini ndizo zinazonufaika zaidi kupitia mtaala wa CBE ikilinganishwa na shule za mashinani, akiwataka viongozi kuwa msitari wa mbele kuhakikisha wanafunzi katika shule hizo pia wanazingatiwa.
“Naomba serikali kuwekeza zaidi kwenye elimu ya watoto hasa maeneo ya mashinani ambako kuna changamoto nyingi za ukosefu wa vifaa vinavyostahili kufanikisha mtaala huu wa CBE. Mambo kama vile mitandao na maabara ni ndoto huku na tunatarajia kwamba hawa watoto wawe viwango sawa na wale wa maeneo ya mijini,” alisema Bi. Kendagor.
Kauli yake ilisisitizwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo Christine Cheboi ambaye aidha aliitaka serikali kuongeza madarasa ya wanafunzi wa shule ya sekondari msingi JSS, ili kuwapa fursa wanafunzi wanaojiunga na kiwango hicho kuendeleza masomo ikizingatiwa uhaba wa shule eneo hilo.
“Tukifika gredi ya sita wanafunzi wanaenda kujiunga na shule zingine, na tumeomba serikali kutuongezea madarasa ya JSS ili wasiache masomo, kwa sababu shule zingine kutoka hapa ziko mbali sana, na watoto wanaweza kuacha masomo baada ya gredi ya sita,” alisema Bi. Cheboi.
