Wadau waelezea kuridhishwa na mwelekeo wa elimu Pokot Magharibi

Na Benson Aswani,
Wadau wa elimu kaunti ya Pokot magharibi wameelezea kuridhishwa na idadi kubwa ya wazazi katika kaunti hiyo ambao wamekumbatia elimu kwa wanao ikilinganishwa na miaka ya awali.
Wakiongozwa na mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Totum Philip Kemei, wadau hao walisema wazazi sasa wamefahamu umuhimu wa elimu kwa wanao kutokana na juhudi ambazo zimeendelezwa na wadau mbali mbali kuwahamasisha wazazi kuhusu umuhimu wa elimu.
Aidha Kemei alitoa wito kwa viongozi kuimarisha miundo mbinu katika shule za kaunti hiyo ili kuboresha mazingira ya kusomea wanafunzi, akisema kwamba hali hiyo itawapelekea wazazi wengi kuwapeleka wanao shuleni.
“Wazazi wa eneo hili hawakuwa wamezingatia maswala ya elimu miaka ya nyuma lakini sasa wamefahamu umuhimu wa elimu na wameikumbatia. Kuimarishwa miundo msingi ya elimu pia kumepelekea hatua hii,” alisema Kemei.
Wakati uo huo Kemei alisema kwamba japo bado kunashuhudiwa visa vya mimba za utotoni miongoni mwa wanafunzi wa kike kaunti hiyo, visa hivi vimepungua pakubwa kufuatia mikakati ambayo imewekwa na serikali kwa ushirikiano na mashirika ya kijamii.
“Mimba za utotoni miongoni mwa wanafunzi wetu yamepungua pakubwa. Japo kuna visa vichache ambavyo huripotiwa hapa na pale, lakini kwa kiasi kikubwa vimepungua eneo hili,” alisema.