Wachimba migodi Pokot Magharibi watakiwa kulinda ardhi ya wakazi

Na Benson Aswani,
Mbunge wa Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong amelalamikia madhara ambayo yamesababishwa na wachimbaji madini eneo la Lami nyeusi katika ardhi ya eneo hilo.


Akizungumza katika kikao kilichowaleta pamoja wakazi na wawekezaji ambao wanaendeleza shughuli ya uchimbaji madini, Lochakapong alisema baadhi ya wachimba madini waliotangulia waliondoka bila ya kufunika machimbo waliyotumia hali ambayo imesalia changamoto kwa wakazi wa maeneo hayo.


“Haja yangu kubwa ni kwamba hii ardhi ya watu wetu ambayo imeharibiwa iweze kufunikwa. wachimbaji madini ambao walitangulia hapa waliacha mashimo ambayo walitumia na sasa wananchi hawawezi kuitumia tena ardhi hii,” alisema Lochakapong.


Hata hivyo, mwekezaji ambaye anaendeleza shughuli ya uchimbaji madini eneo hilo Okech Salah amewahakakishia viongozi na wakazi wa eneo hilo kwamba atachukua jukumu la kuhakikisha hali hiyo inashughulikiwa, kando na kuendeleza miradi ya kuwanufaisha wakazi.


“Tutatumia fedha zetu kuziba haya mashimo ambayo yalichimbwa na walanguzi wa dhahabu. Nawahakikishia hilo, na mkitaka kujua kwamba sisemi uongo, mimi nimeanza kusaidiana na watu wa Pokot magharibi hata kabla ya kuanza kuchimba madini katika sehemu hii,” alisema Salah


Ni kufuatia hatua hiyo ambapo wakazi wa eneo hilo sasa wameapa kutokubali mwekezaji yeyote ambaye ataanza shughuli za kuvuna madini eneo hilo bila ya kufuata mkondo aliochukua salah wa kuwahusisha wakazi kabla ya kuanza shughuli zake.


Kwa upande wake naibu kamishina eneo la Sigor Philip Mbuvi aliwaonya wazazi eneo hilo dhidi ya kuwahusisha watoto katika shughuli ya uchimbaji madini, na badala yake kuhakikisha kwamba wanahudhuria masomo.


“Ni lazima kila mtoto aende shule. Najua kwamba uchimbaji madini unatuletea pesa. Lakini elimu ni muhimu sana kwa watoto. Wazazi wengi huku wamekuwa wakiwashirikisha watoto wao kwa shughuli ya uchimbaji madini na kupuuza masomo yao. Hebu tuache hayo,” alisema Mbuvi.