Wabunge waendelea kung’ang’ania mkoba wa NG-CDF

Na Benson Aswani,
Viongozi wa kaunti ya Pokot amgharibi wameendelea kutofautiana na pendekezo la kinara wa chama cha ODM Raila Odinga la kutaka hazina ya maendeleo kwa maeneo bunge NG-CDF kuondolewa na badala yake fedha zinazotengewa hazina hiyo kuongezwa kwa mgao wa kaunti.


Wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong, viongozi hao walisema, kamati ya kitaifa ya mazungumzo NADCO iliyoundwa na rais William Ruto na Odinga, ilikusanya maoni ya wananchi kuhusu swala la NG-CDF, na idadi kubwa ya wananchi ikaunga mkono kuendelea kuwepo hazina hiyo.


Aidha, Lochakapong alisema katiba iliyopo kwa sasa inashauri sheria kubuniwa baada ya kuwahusisha wananchi katika vikao vya umma, na maoni ambayo yanatolewa na wananchi katika vikao hivyo yanapasa kupewa kipau mbele.


“Tulikuwa na mkutano wa pamoja wa wabunge wa Kenya kwanza na ODM, kinara wa ODM Raila Odinga akasema kwamba NG-CDF iondolewe. Nataka kumweleza kwamba kamati ya NADCO ilikusanya maoni kutoka kwa wananchi na idadi kubwa ya wananchi wakasema NG-CDF iendelee kuwepo,” alisema Lochakapong.


Wakati uo huo, Lochakapong alisema mahakama ya upeo nchini iliidhinisha kuendelea kuwepo hazina hiyo baada ya kutoa uamuzi kwamba utekelezwaji wa hazina hiyo hauwezi kuhujumu kwa vyovyote utekelezwaji wa ugatuzi mradi imetekelezwa kwa utaratibu unaofaa.


“Hata mahakama ya upeo ilisema NG-CDF haiwezi kwa vyovyote kuathiri utekelezwaji wa ugatuzi, mradi imetekelezwa kwa utaratibu unaofaa. Kwa hivyo wacha tutekeleze kile ambacho wananchi wamekubali kwa sababu hii sheria si ya mtu, ni ya wakenya,” alisema.