Visa vya wizi wa mifugo vyachipuka tena mpakani pa Pokot Magharibi na Turkana

Na Emmanuel Oyasi,
Mbunge wa Kacheliba kaunti ya Pokot magharibi Titus Lotee amelalamikia kukithiri utovu wa usalama mpakani pa eneo hilo na kaunti jirani ya Turkana.


Akizungumza na kituo hiki, Lotee alisema licha ya serikali ya kitaifa kupitia idara ya usalama kuendesha oparesheni ya kutwaa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria, wakazi katika baadhi ya maeneo ya kaunti ya Turkana wangali wanamiliki silaha hizo hali ambayo imechangia uvamizi wa kila mara wakazi wa Pokot magharibi wakipoteza mifugo wao.

“Tangu sisi kama jamii ya Pokot kukubali kusalimisha silaha haramu na kukubali kuishi kwa amani, tunasikitika kwamba watu wamesalia masikini eneo la Kacheliba, kwa sababu jirani zetu wangali na bunduki ambazo wanatumia kuiba mifugo wetu,” alisema Lotee.


Lotee sasa anataka serikali kuwafidia wakazi ambao wamepoteza mifugo wao mikononi mwa wavamizi kwani wengi wao wamesalia katika hali ya umasikini ikizingatiwa wakazi wengi wanategemea mifugo kwa uchumi.


Wakati uo huo Lotee alitaka kubuniwe sheria ambayo itashinikiza kutwaliwa mali ya eneo ambako mifugo walioibwa wameelekea hadi watakapopatikana kama njia moja ya kulinda mali ya wakazi.


“Jambo la kwanza ningeomba, watu ambao wamepoteza mali yao yote, ni lazima serikali iwafidie. Jambo la pili, kuundwe sheria ambayo itasaidia kurejesha mifugo wanaoibwa, ambapo mifugo wakiibwa, mali ya sehemu ambako wameelekea itwaliwe hadi watakaporejeshwa,” aliongeza.