Viongozi watakiwa kujitenga na siasa na kuwahudumia wananchi

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ametoa wito kwa viongozi kushirikiana katika kuhakikisha kwamba wakazi wa kaunti hii wanapokea huduma bora.
Akizungumza katika hafla moja mjini Kapenguria, gavana Kachapin alisema ni jukumu la kila kiongozi kutumia nafasi ambayo anashikilia kwa sasa kuona kwamba anatoa huduma zinazostahili kwani ndilo jukumu kuu la uongozi.
Aliwasuta viongozi wa kisiasa ambao wanaendeleza siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, akisema sasa si wakati wa kuendeleza siasa bali ni wakati wa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maisha bora kutokana na huduma ya viongozi.
“Tushirikiane tuone tumesaidia watu wetu. Kila mtu sasa amepewa nafasi na kila mmoja anapasa kutumia nafasi yake kuhakikisha watu wetu wanapata huduma zinazofaa. Hakuna haja tuanze kupigania mambo ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema Gavana Kachapin.
Wakati uo huo gavana Kachapin alitoa wito kwa wadau mbali mbali kutumia kipindi hiki ambapo kunashuhudiwa mvua kuwashinikiza wananchi kuhusika shughuli za kilimo ili kuafikia usalama wa chakula katika kaunti hiyo.
“Mungu ametubariki na mvua ya kutosha, na sasa viongozi tunapasa kutumia nafasi hii kuwashinikiza wananchi kutumia mvua hii kuendeleza kilimo ili tuwe na chakula cha kutosha,” alisema.
