Viongozi washutumu kuchipuka tena utovu wa usalama mipakani pa Pokot na Turkana

Na Benson Aswani,
Viongozi kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kushutumu visa vya mauaji ambavyo vimeshuhudiwa mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana katika siku za hivi karibuni.
Wa hivi punde kuzungumzia swala hilo ni mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto ambaye alitaka vitengo husika kuchukua hatua za haraka na kufanya uchunguzi ambao utapelekea kunaswa wahalifu wanaoendeleza uovu huu ili kurejesha utulivu maeneo hayo.
Aidha Moroto aliwasuta maafisa wa kitengo cha kukabili wizi wa mifugo kwa kile alisema kuzembea katika majukumu yao, akidai wamekuwa wakipuuza malalamishi ya wakazi wanaoibiwa mifugo yao hali ambayo imezidisha visa hivi.
“Tunataka serikali ichunguze vizuri. Mtu ako kwenye barabara pekee, hana chochote halafu anapigwa risasi. Ni uchungu! Kwa hivyo ni lazima haki itendeke. Na hawa askari wa ASTU wamekuwa chanzo cha kuongezeka visa hivi. Watu wakikimbia kwao kuripoti wizi wa mifugo, wanawapuuza tu,” alisema Moroto.
Wakati uo huo Moroto alielezea mipango ya kukutana viongozi kutoka pande zote mbili utakaotumika kuangazia hali ya usalama ili kupata suluhu kwa tatizo hili la muda mrefu, na kuwapa wakazi mazingira salama hasa kwa wanafunzi wanaoendelea na mitihani ya kitaifa.
“Tutaitana hivi karibuni na viongozi tuweze kuchunguza visa hivi, kwa sababu tunataka amani, tunataka watoto wetu wasome, na hasa wakati huu ambapo wanaendelea na mitihani ya kitaifa,” alisema.
