Viongozi waendelea kutuma risala za rambi rambi kufuatia kifo cha Raila Odinga

Na Benson Aswani,
Viongozi mbali mbali nchini wameendelea kuomboleza kifo cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ambaye aliaga dunia mapema jana akiwa nchini India.
Gavana wa kaunti ya Pokot Magharibi Simon Kachapin amewaongoza viongozi katika kaunti hii kutuma risala za rambi rambi kufuatia kifo cha kiongozi huyo wa siasa za upinzani.
Gavana kachapin alimtaja odinga kuwa kiongozi shupavu na kwamba kifo chake ni pigo kwa taifa hili kufuatia mchango wake mkubwa kwa ustawi wa demokrasia nchini.
“Tumepata kwa mshutuko kifo cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga tukikumkumbuka kama shujaa mkubwa sana katika taifa hili letu. Yeye ndiye alipigania demokrasia, haki za binadamu na uhuru ambao tuko nao kwa sasa,” alisema Gavana Kachapin.
Kachapin alisema kiongozi huyo wa upinzani amefanya mengi ambayo hayawezi kuhesabika haswa katika gatuzi hilo la Pokot magharibi.
“Raila si mtu ambaye unaweza sema alifanya hili na hili katika sehemu moja. Huyu ni mtu ambaye alikuwa shujaa wa kitaifa, na kaunti hii ya Pokot magharibi ni moa ya kaunti ambazo zilinufaika sana na harakati zake,” alisema.
Kwa upande wake aliyekuwa seneta wa kaunti hiyo Samwel Poghisio alisema taifa limepoteza mtu ambaye alitegemewa sana katika siasa za taifa hili, ikizingatiwa alichangia pakubwa katika demokrasia ya nchi enzi za uhai wake.
“Nimesikitika sana kupata habari hizi kwamba tumempoteza mtu ambaye amekuwa rafiki wa karibu na mtu ambaye tulikuwa tukimtegemea sana katika siasa za taifa hili, na ambaye alikuwa kichocheo kikubwa kwa demokrasia ya taifa,” alisema Poghisio.
Poghisio alisema Raila alipenda sana historia ya kaunti hii ya Pokot magharibi akiwa ametangamana na viongozi mbali mbali kutoka kaunti hiyo licha ya kwamba alikuwa katika mrengo wa upinzani nyakati hizo.
Aidha Poghisio alisema Raila amechangia pakubwa katika maendeleo ya kaunti, ikiwemo kuanzisha barabara mbali mbali katika maeneo ambayo hayakuwa na barabara wakati akihudumu kama waziri wa barabara.