Viongozi waelezea haja ya kudhibitiwa shughuli ya uchimbaji madini Masol

Na Benson Aswani,
Mbunge wa Sigor kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong ametaka shughuli ya uchimbaji madini eneo la Masol Kudhibitiwa.
Akizungumza baada ya kikao cha kubuni mikakati ya kuweka kamati itakayosimamia maswala ya ardhi eneo hilo, Lochakapong alisema uchimbaji madini usiodhibitiwa utapelekea uharibifu wa ardhi na hasa maeneo ya malisho ikizingatiwa wengi wa wakazi eneo hilo ni wafugaji.
Aidha Lochakapong alisema kamati ambayo itabuniwa itasaidia katika kuwaelekeza watu wanaotafuta madini maeneo ambayo wanapasa kuendeleza shughuli hiyo ili kuzuia uchimbaji wa madini usio na taratibu zinazohitajika.
“Kuna watu wengi wamekuja sehemu hii kwa sababu ya uchimbaji wa madini. Na jinsi wanakuja, hawafuati sheria yoyote. Na hivyo wasipodhibitiwa, watakuja kuharibu eneo hili ikizingatiwa wengi wa wakazi wanategemea sehemu hii kwa malisho,” alisema Lochakapong.
Kauli yake imesisitizwa na viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Masol Wilson Chekeruk ambao walisema wakazi wengi watanufaika na shughuli hiyo ya uchimbaji madini iwapo itaweza kudhibitiwa.
“Madini ni raslimali kubwa ambayo Mungu ametupa eneo hili. Kwa kubuni kamati ya kudhibiti shughuli hii kutasaidia pakubwa kwa watu wetu kunufaika na shughuli hii,” alisema Chekeruk.
