VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATISHIA KUMBANDUA KINDIKI AFISINI.

Mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto na mwenzake wa Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi Titus Lotee wamesuta hatua ya kuagizwa kuandikisha taarifa na idara ya DCI jijini Nakuru kufuatia swala la utovu wa usalama kaskazini mwa bonde la ufa.

Wakizungumza muda mfupi tu baada ya kuandikisha taarifa hiyo jumatatu, viongozi hao miongoni mwa viongozi wengine walioandamana nao, walimsuta pakubwa waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kwa kile walidai matumizi mabaya ya afisi.

Viongozi hao walimtaka rais William  Ruto kumbadilishia majukumu waziri Kindiki la sivyo waanzishe mchakato wa kumng’oa afisini kwa kile walidai matumizi mabaya ya afisi.

“Kuna mawaziri ambao hawaelewi kazi yao. Sisi tulihusika pakubwa katika kuiweka serikali hii mamlakani. Hivyo tuna haki pia ya kudai haki zetu. Tunamtaka rais kumbadilishia majukumu waziri wa usalama Prof. Kithure Kindiki la Sivyo sisi tutaanzisha mchakato wa kumwondoa afisini kwa sababu anatumia vibaya afisi.” Walisema.

Aidha Viongozi hao waliisuta serikali kwa kushindwa kushughulikia swala la usalama kaskazini mwa bonde la ufa hali ambayo imelemaza miradi ya maendeleo eneo hili, na badala yake kuendelea kuwahangaisha viongozi ambao wanatetea maslahi ya wananchi.

“Kama viongozi tumewasilisha mahitaji yetu kwa muda lakini hamna lolote ambalo limetekelezwa hadi kufikia sasa. Kile ambacho sasa serikali inafanya ni kuwahangaisha viongozi wa kaunti hii ambao wanajaribu kuwatetea wananchi ambao wameathirika zaidi na utovu wa usalama.” Walisema.

Na Emmanuel Oyasi.