Viongozi Pokot Magharibi watakiwa kuandaa kikao cha kuangazia swala la uchimbaji madini

Na Emmanuel Oyasi,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio amewataka viongozi kaunti hiyo kuandaa kikao cha kujadili hatima ya shughuli ya uchimbaji madini ambayo ilisitishwa kwa muda na serikali baada ya kuripotiwa maafa katika baadhi ya migodi.


Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na kituo hiki, Poghisio alisema inasikitisha kwamba viongozi wote wamesalia kimya kuhusu swala hilo licha ya kwamba familia nyingi zimepoteza wapendwa wao kupitia shughuli hiyo ya uchimbaji madini.


Poghisio aidha alishutumu kile alidai baadhi ya viongozi kutumia nafasi yao kunufaika na shughuli hiyo ya uchimbaji madini licha ya kusitishwa, akitaka kuendelezwa zoezi la kuhusisha umma kuhusu jinsi shughuli hiyo itakavyorejelewa kabla ya kurejelewa rasmi.


“Inabidi watu wasemezane, si kwamba mtu mmoja au wawili wanaamua kuhusu maswala ya uchimbaji wa migodi. Ningependa sana viongozi tuje pamoja na tuangazie jinsi jamii zilizowapoteza watu wao zitashughulikiwa,” alisema Poghisio.


Poghisio alishutumu kile alisema siasa za mapema na za kuegemea mirengo ambazo zinaendelezwa na viongozi katika kaunti hiyo, akisema zimepelekea migawanyiko miongoni mwa viongozi hali ambayo imefanya vigumu kwao kukutana na kuangazia changamoto za wakazi.


“Hizi siasa za mapema ambazo viongozi wanafanya zinaleta migawanyiko ambapo hatupati nafasi ya kuketi na kuangazia changamoto ambazo watu wetu wanakumbana nazo,” alisema.