Viongozi Pokot magharibi walaani kuchipuka tena utovu wa usalama mpakani pa Pokot na Turkana

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya pokot magharibi simon kachapin amelaani mauaji ya watu watatu waliopigwa risasi katika kijiji cha Loperumoi, Morita–Rumos, mpakani pa kaunti hiyo na ile ya Turkana.


Gavana kachapin aliwataka wakazi kwenye maeneo hayo kudumisha utulivu na kutojihusisha na ulipizaji kisasi kutokana na mauaji ya wanamme hao watatu.


Gavana kachapin aidha aliwaonya viongozi hasaa wa kisiasa dhidi ya kuendeleza uchochezi akisema kwamba jamii ya Pokot na Turkana zimekua zikiishi pamoja kwa mda mrefu.


“Jamii zetu zimeishi tangu jadi, na zitaendelea kuishi. Tupende tusipende sisi ni majirani, na itakuwa vibaya sana kama viongozi ndio watakuwa wanachochea utovu wa usalama,” alisema Gavana Kachapin.


Wakati uo huo gavana Kachapin aliitaka serikali kuchukua hatua za haraka na kurejesha utulivu huku pia akitoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa pamoja wa viongozi kutoka kaunti hizo mbili.


“Nataka nitoe wito kwa serikali kuu ambayo tunajua wapo na uwezo wa kuleta amani katika sehemu hizo. Na pia kama viongozi tutahitajika kuona kwamba tunakutana na kuongea ili tukomeshe uhalifu huu,” alisema.


Baadhi ya viongozi katika kaunti hiyo ya Pokot Magharibi wakiongozwa na naibu spika Victor Siywat walishutumu vikali matamshi yaliyotolewa na gavana wa kaunti ya Turkana Jeremia Lomurkai kuhusu visa vya uvamizi ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa mipakani pa kaunti hizo mbili.


Walidai visa vya utovu wa usalama vimeendelea kuripotiwa kwenye mipaka ya kaunti hizo kutokana na matamamshi ya kiholela kutoka kwa viongozi hao ila inasikitisha kwamba idara husika haijachukua hatua zinazofaa kukomesha hulka hiyo.


“Viongozi kutoka ule upande mwingine wakiongozwa na gavana, wamekuwa msitari wa mbele kueneza matamshi ya chuki ambayo yamekuwa yakikochea utovu wa usalama baina ya jamii za kaunti hizi mbili,” alisema Siywat.