VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAISUTA SERIKALI KWA KUWAHANGAISHA WAKAZI WA ARDHI YA CHEPCHOINA.
Na Emmanuel Oyasi.
Baadhi ya viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameisuta serikali ya Kenya kwanza kwa kutokuwa makini katika kushughulikia masaibu ambayo yanawakumba wakazi waliofurishwa katika ardhi yenye utata ya Chepchoina mpakani pa kaunti hii na kaunti jirani ya Trans nzoia.
Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto na mwenzake wa Sigor Peter Lochakapong, viongozi hao walisema kinyume na serikali zilizotangulia, ni katika serikali hii ambapo wakazi katika ardhi hiyo wamepitia mahangaiko kutokana na kile walisema utepetevu miongoni mwa maafisa husika.
Viongozi hao aidha waliwasuta maafisa wa usalama kwa kutumika kuwahangaisha wananchi ambao walisema walipewa ardhi hizo kwa njia halali na rais mustaafu hayati Daniel Moi katika utawala wake akiwa rais.
“Watu wanaoishi kwenye ardhi ya Chepchoina si jamii ya Pokot pekee bali hata jamii ya Turkana na Marakwet. Na watu hawa walipewa ardhi hizi na hayati Moi. Lakini serikali hii imekuwa ikiwahangaisha wakazi na sasa wanafurushwa na polisi ambao ushuru wanaotoa watu hawa ndio unaowalipa mishahara.” Alisema Moroto.
Viongozi hao sasa wanaitaka serikali kupitia idara ya ardhi kushughulikia utata huo na kuhakikisha kwamba wakazi ambao wamefurushwa katika ardhi zao wanatendewa haki kwani wanamiliki ardhi hizo kwa njia ya halali.
Aidha walitaka uchunguzi kufanywa na kuchukuliwa hatua maafisa wote wa serikali ambao wamehusika katika kuwasababishia wakazi wa ardhi hizo mahangaiko.
“Wale wanaohusika na mashamba kwenye serikali hii wafanye haki. Kwa sababu kuna watu ambao walipewa ardhi kwa njia halali na hawa hawapasi kudhulumiwa. Uchunguzi unapasa kufanywa na iwapo kuna maafisa wa serikali ambao wametumia vibaya afisi zao, wachukuliwe hatua.” Alisema Lochakapong.