Vijana watakiwa kujitosa kwenye kilimo na kutotegemea kazi za afisini

Na Benson Aswani,
Wito umetolewa kwa vijana katika kaunti ya Pokot magharibi kujitosa katika kilimo ili kujipatia riziki za kila siku badala ya kutegemea kuajiriwa katika kazi za afisini ambazo zimekuwa nadra kupatikana katika enzi hizi.
Akizungumza baada ya hafla ya kutoa mafunzo kwa wakulima kaunti hiyo kwenye mkahawa mmoja mjini Makutano, afisa wa mahusiano kwenye mpango wa Tupande one acre fund Job Kinyale, alisema kilimo kina faida kubwa na hakipasi kuchukuliwa kama chaguo la pili baada ya kukosa kazi za afisi.
Wakati uo huo kinyale aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kujihusisha na kilimo cha mimea ambacho alisema kinafanya vyema katika kaunti hiyo, na kutoegemea tu kilimo cha mifugo ambacho huwa na changamoto hasa nyakati za kiangazi.
“Tumeona kwamba vijana huchukulia kilimo kama chaguo la pili hasa baada ya kukosa ajira za afisini. Lakini tumeona uzuri wa kilimo na tunajaribu kufanya kile kinaitwa kubadilisha mtazamo, ili vijana hawa wasione kilimo kama kazi ya wazee bali wakione kama kazi itakayowapa mapato,” alisema Kinyale.
Ni wito ambao ulikaririwa na baadhi ya vijana wakulima ambao walihudhuria mafunzo hayo wakiongozwa na Mika Limo.
Aidha vijana hao waliyataja mafunzo hayo kuwa yenye manufaa makubwa katika kuendeleza shughuli zao za kilimo.
“Nitawaeleza vijana kwamba kazi za afisini haziwezi kututosheleza sote, ila kilimo pia kinalipa. Mimi kama kijana sijaajiriwa ila sijashindwa kujisismamia kifedha kutokana na kilimo,” alisema Limo.
