Usimamizi mbaya wa raslimali ndio unaohujumu maendeleo ya taifa; Kachapin

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amesema maono ya rais kulifanya taifa hili kuwa miongoni mwa mataifa ambayo yameimarika kiuchumi yani first world countries yataafikiwa iwapo kutakuwepo na usimamizi bora wa raslimali za taifa.


Akizungumza katika hafla moja mjini Makutano, Kachapin alisema taifa hili lina raslimali nyingi ambazo iwapo zitasimamiwa vyema na kutumika jinsi inavyopasa zinaweza kuimarisha pakubwa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Gavana Kachapin alisema tatizo kubwa ambalo taifa hili linakabiliwa nalo ni usimamizi mbaya wa raslimali za umma, hali ambayo inapelekea taifa kutoimarika kiuchumi kwa kasi inayotarajiwa, huku idadi kubwa ya wananchi wakiendelea kuishi maisha ya ufukara.


“Maono aliyo nayo rais kuhusu kulifanya taifa hili kuimarika kiuchumi na kufikia viango vya mataifa ya first world countries, yatawezekana tu kama viongozi tutasimamia vyema raslimali ambazo zinapatikana hapa nchini,” alisema Gavana Kachapin.


Wakati uo huo Kachapin alitoa wito kwa viongozi katika ngazi za kaunti kuchangia katika juhudi za kuhakikisha malengo ya rais kupandisha hadhi ya taifa hili yanaafikiwa kwa kuhakikisha raslimali zinazopatikana nchini zinatumika vyema.


“Kama magavana tunapasa kubadilisha mambo hata kama ni kwa njia ndogo tuwezavyo, kwa sababu mimi nikifanya kidogo, mwingine afanye kidogo, nchi hii itafika first world ambayo rais anasema. Hatuwezi kusubiri tu kwamba rais afanye kila kitu,” alisema.