Ushirikiano kati ya kamishina na serikali ya kaunti ya Pokot magharibi watajwa kuwa chanzo cha kupungua uhalifu

Na Benson Aswani,
Naibu gavana kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole ametaja ushirikiano baina ya kamishina wa kaunti hiyo Abdulahi Khalif na uongozi wa gavana Simon Kachapin kuwa ndio umechangia kupungua pakubwa visa vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa mipakani pa kaunti hiyo.
Akizungumza katika hafla moja, Komole alisema ikilinganishwa na watangulizi wake, visa vya utovu wa usalama ambavyo vimekuwa kero kwa miaka mingi maeneo hayo vimepungua pakubwa katika kipindi cha kamishina wa sasa kufuatia ushirikiano wake na serikali ya kaunti.
Aidha Komole alisema hatua ya serikali ya kaunti kujenga vituo vya polisi katika baadhi ya maeneo ambako kumekuwa kukishuhudiwa visa hivi imechangia kuhakikisha wakazi wa maeneo haya wanaishi kwa amani na kuendeleza shughuli zao za maisha.
“Pongezi zinamwendea kamishina wa kaunti hii Abdulahi Khalif kwa sababu ameshirikiana kwa karibu na serikali ya gavana Kachapin, hali ambayo imepelekea kupungua pakubwa visa vya uvamizi kwenye mipaka ya kaunti hii,” alisema Komole.
Kwa upande wake aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo John Lonyangapuo amependekeza wahalifu wanaoendeleza wizi wa mifugo kupatiwa mafunzo na kuajiriwa katika kikosi cha usalama kama njia moja ya kutokomeza visa hivi, swala alilodai lilijaribiwa enzi za hayati rais Daniel Moi na kuzaa matunda.
“Hawa wezi wenye wako kwenye mipaka ya kaunti hii wamejifundisha kutumia silaha. Kuna hasara kwa wao kuchukuliwa na kupewa mafunzo ili wapewe kazi ya kulinda nchi? Ni mbinu ambayo ilitumika na hayati rais Moi na ikazaa matunda,” alisema.