Uchimbaji madini watajwa kuwa chanzo cha utovu wa usalama mipakani pa Pokot Magharibi na Turkana


Na Benson Aswani,
Baadhi ya viongozi wa kaunti ya Pokot magharibi sasa wanadai kwamba shughuli ya uchimbaji madini hasa maeneo ya mipakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana ndiyo imechangia visa vya utovu wa usalama maeneo hayo.

Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto na mwenzake wa Sigor Peter Lochakapong, viongozi hao walidai kwamba kabla ya kuanza shughuli ya uchimbaji madini maeneo hayo ya mipakani, jamii za pokot na Turkana zilikuwa zikiishi kwa amani na kutangamana bila ya mizozo.


“Mbeleni jamii za Pokot na Turkana zilikuwa zikiishi pamoja wakifanya mambo yao kwa umoja bila mizozo. Lakini tangu maswala ya kuchimba madini yalipoingia, tukaanza kushuhudia mauaji na mizozo kati ya jamii hizi,” alisema Moroto.


Aidha viongozi hao walidai kwamba maafisa wa akiba NPR wanatumika visivyo kulinda shughuli za kibiashara za wawekezaji badala ya kulinda wakazi wa maeneo hayo na mali zao.


Walidai baadhi ya visa vya uvamizi vimeshuhudiwa maeneo ambako kuna maafisa wa NPR ila wakaondolewa na kupelekwa kulinda mali za wawekezaji na kutoa mwanya kwa wahalifu kutekeleza mauaji ya raia.


“Biashara ni nzuri ila isiwe chanzo cha matatizo baina ya jamii. Wale NPR ambao tumepewa na serikali, badala ya kulinda wananchi na mali yao, sasa wamekuja kulinda biashara za wale ambao wanajiita wawekezaji. Hilo hatutakubali kama viongozi eneo hili,” alisema Lochakapong.