Uchimbaji madini ulituletea hasara kubwa na haufai kuruhusiwa tena kiholela; Moroto

Na Emmanuel Oyasi,
Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kulalamikia madhara ambayo yalisababishwa na shughuli ya uchimbaji madini iliyokuwa ikiendeshwa maeneo kadhaa ya kaunti hiyo bila kufuata taratibu.


Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, viongozi hao walisema shughuli hiyo ilipelekea maafa ya wakazi wengi kufuatia hatua ya wawekezaji waliokuwa wakichimba madini kutojali usalama wa wakazi wakati wakiendeleza shughuli hiyo.


Moroto alisema ni kutokana na hali hiyo ambapo viongozi katika kaunti hiyo walishinikiza kusimamishwa shughuli hiyo hadi taratibu zote za uchimbaji madini zitakapozingatiwa, na kuhakikisha kwamba walioathirika wanapata haki.


“Ukienda lami Nyeusi, Kambi karai na Turkwel kumeharibika sana, lakini nashukuru viongozi kwa sababu tumechukua jukumu la kusimamisha. Kuna maafa yaliyotokea maeneo hayo ila wahusika hawakujali hata kufidia jamii za waathiriwa. Na hivyo tukasema haiwezekani tena,” alisema Moroto.


Aidha Moroto aliendelea kutoa wito kwa wizara ya madini kuhakikisha kwamba sheria za uchimbaji madini zinazingatiwa kwa mwekezaji yeyote ambaye ataingia kaunti hii kutekeleza shughuli ya uchimbaji madini ili kuhakikisha usalama wa wakazi pamoja na kulinda raslimali za kaunti kwa ujumla.


“Tumeiomba wizara ya madini kuhakikisha kwamba kuna utaratibu wa jinsi ya kuendeleza shughuli ya uchimbaji madini, na sheria zote zizingatiwe kwa yeyote ambaye atakuja kuchimba dhahabu katika kaunti hii, ili tuhakikishe usalama wa watu wetu,” alisema.