Shule ya upili ya Tartar yafungwa ghafla kufuatia maandamano ya wanafunzi

Wanafunzi wa shule ya upili ya Tartar wakiwa nje ya afisi ya mkurugenzi wa elimu, Picha/Benson Aswani

Na Benson Aswani,
Shule ya upili ya Tartar kaunti ya Pokot magharibi imefungwa kwa muda usiojulikana ili kutoa nafasi kwa uongozi wa shule hiyo na idara ya elimu kuangazia malalamishi ambayo wanafunzi wa shule hiyo waliibua dhidi ya uongozi wa shule.


Wanafunzi wa shule hiyo waliandamana alhamisi wiki hii hadi afisi za tume ya huduma za walimu TSC kuwasilisha lalama zao dhidi ya shule hiyo, mkurugenzi wa elimu kaunti hiyo Simon Wamae akiwahakikishia kwamba lalama zao zitaangaziwa kikamilifu.


Wamae alisema malalamishi ya wanafunzi hao yana uzito na ni sharti yaangaziwe kwa ukamilifu.
“Tunawapongeza kwa kuja katika afisi hii, na tunawaahidi kwamba tutaangazia kikamilifu malalamishi yenu kwa sababu tumeyasikiliza na kuona kuwa yana uzito ambao unafaa kuangaziwa,” alisema Wamae.


Kauli yake ilisisitizwa na naibu mkurugenzi wa tume ya huduma kwa walimu TSC kaunti hiyo John Paul Wepoe ambaye alisema watamwita mwalimu mkuu wa shule ya Tartar ili kusikia upande wake kabla ya kufanya maamuzi.


“Tumethibitisha kuwa baadhi ya malalamishi yenu ni kweli hata kabla ya kumaliza majadiliano. Kwa hivyo tutamsikiliza mwalimu mkuu tupate upande wake kabla ya kuchukua hatua,”alisema Wepoe.


Baadhi ya malalamishi ambayo wanafunzi hao waliwasilisha kwa tume ya huduma kwa walimu TSC dhidi ya mwalimu mkuu ni pamoja na uongozi mbaya, kupelekea matokeo mabaya ya shule katika mitihani ya kitaifa, kuwadhulumu walimu, ukosefu wa maji safi shuleni, chakula duni miongoni mwa maswala mengine.