Shinikizo za kutaka shule za JSS kujisimamia zaendelea kutolewa na vyama vya walimu

Na Benson Aswani,
Chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri KUPPET kimeshikilia msimamo wake kwamba ni lazima serikali itenganishe shule za sekondari msingi JSS na shule za msingi.


Katika mkao na wanahabari, katibu mkuu wa chama hicho tawi la Pokot magharibi Alfred Kamuto alidai kwamba shule za JSS zinapitia changamoto nyingi chini ya usimamizi wa shule za msingi, kwani fedha ambazo zimekuwa zikitengewa shule hizo zinatumika vibaya na walimu wakuu wa shule za msingi.


“Fedha ambazo zinatengewa shule za JSS zimekuwa zikitumika vibaya na walimu wakuu wa shule za msingi. Na kama chama cha KUPPET tunasema shule za JSS zinafaa kujisimamia ili kuwe na matumizi mema ya raslimali zinazotengewa shule hizo,” alisema Kamuto.


Kauli yake ilisisitizwa na naibu mwenyekiti wa chama hicho kaunti hiyo Anthony Merisia, ambaye alisema inasikitisha kuona kwamba baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi wanalazimika kuendeleza masomo yao chini ya miti kutokana na ukosefu wa madarasa.


“Kama tunataka elimu bora, ni lazima shule za JSS zitenganishwe na shule za msingi kwa sababu tunavyozungumza, baadhi ya wanafunzi bado wanaendeleza masomo yao chini ya miti, na eti tunaziita shule za sekondari msingi,” alisema Merisia.


Kwa upande wao walimu wa JSS kaunti hiyo wakiongozwa na msemaji wao Geofrey Doiwan waliitaka serikali kuwaajiri kwa mkataba wa kudumu walimu wa nyanjani, wakitaka swala la walimu kuhudumu kama walimu wa nyanjani kufutiliwa mbali.


“Serikali inafaa kuondoa kabisa hili swala la walimu wa nyanjani kwa sababu walimu wote wamehitimu, na hawa walimu wanaotajwa kuwa wa nyanjani wanafanya kazi sawa na walimu walioajiriwa rasmi,” alisema Doiwan.


Chama hicho cha KUPPET kilisema kitalazimika kuwaondoa madarasani walimu wa JSS iwapo serikali haitatimiza masharti yao.