Shilingi bilioni 1.16 zatengwa kukamilishwa mradi wa maji wa Siyoi-Muruny

Na Benson Aswani,
Waziri wa maji Erick Muuga ameahidi kuharakishwa mradi wa maji wa Siyoi-Murunyi ili kutatua changamoto ya uhaba wa maji kwa wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi ambao wamesubiri wa miaka mingi kukamilishwa mradi huo.


Akizungumza mjini Kapenguria baada ya kukagua mradi huo, Muuga alisema tayari shilingi bilioni 1.16 zimetengwa katika bajeti ya kipindi cha mwaka wa kifedha 2026/2027 ambazo zitatumika kukamilisha mradi huo ambao umefikia asilimia 87.


“Niliahidi kwamba ni lazima huu mradi wa maji wa Siyoi-Muruny ukamilike, na ili kuhakikisha hili linafanyika, tayari shilingi bilioni 1.16 zimetengwa kwa ajili ya mradi huo ambao unalenga kusuluhisha tatizo la maji kwa mkazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi,” alisema Muuga


Waziri Muuga alisema serikali ya rais William Ruto imejitolea kuhakikisha kwamba hamna eneo lolote nchini ambalo linasalia nyuma inapokuja katika utekelezwaji wa miradi ya maendeleo.


“Kama serikali tumejitolea kuhakikisha kwamba hamna sehemu yoyote ambayo itasalia nyuma kimaendeleo,” alisema.


Wakati uo huo Muuga amemtaka mwanakandarasi ambaye anaendeleza mradi huo kuhakikisha kwamba unatekelezwa na kukamilika ndani ya kipindi ambacho kiliwekwa.


“Nimemwagiza mwanakandarasi anayeendelea mradi huo kuhakikisha kwamba zipo raslimali za kutosha na kuuharakisha ili ukamilike katika kipindi ambacho kimewekwa,” alisema.