Serikali ya Pokot magharibi yaendesha vikao vya kukusanya maoni kuhusu bajeti

Na Benson Aswani,
Maswala ya elimu na afya yalipewa kipau mbele katika shughuli ya kuwahusisha wananchi kutoa maoni yao kuhusu maswala ambayo yanapasa kupewa kipau mbele wakati wa kuunda bajeti ya mwaka 2027/2028 kaunti ya Pokot magharibi.


Wakizungumza katika shughuli hiyo ambayo iliandaliwa kwenye ukumbi wa Mtelo mjini Kapenguria, wakazi hao wakiongozwa na Alvin Lusaji kutoka shirika la Now and Beyond, walisema serikali inapasa kutenga fedha za kutosha katika idara ya elimu ili kuhakikisha usawa kwa wakazi wote.

“Ili tuweze kuendelea, ni lazima kila familia ifikie elimu. Serikali inapasa kuwekeza kikamili katika elimu ili hata familia ambazo hazina uwezo kifedha zipate kuwaelimisha watoto wao,” alisema Lusaji.


Aidha walipendekeza kuongezwa mgao wa idara ya afya hadi asilimia 35 ya bajeti ikizingatiwa kwamba imegatuliwa kikamilifu kwa serikali za kaunti.


“Tunasihi sana serikali kuongeza raslimali katika idara ya afya ili angalau ifikie asilimia 35, kwa sababu idara ya afya imegatuliwa kikamilifu kwa serikali za kaunti na ni pana sana ikilinganishwa na idara zingine zilizogatuliwa,” alisema.


Aidha wakazi hao hasa vijana walitaka serikali kuhakikisha kwamba vituo vya kuwawezesha vijana vinawekwa vifaa vya kutosha ili kuwawezesha kuwekeza katika ubunifu na kujiundia nafasi za ajira.


“Tunataka hivyo vituo vya kuwawezesha vijana kuwekwa vifaa vya kutosha ambavyo vitawawezesha vijana kuwa wabunifu,” alisema.


Walitaka mapendekezo ambayo yametolewa kupewa kipau mbele wakati wa kuunda bajeti hiyo.