Serikali ya kaunti yatoa hundi ya shilingi milioni 19 kwa makundi ya wakulima Karas

Na Benson Aswani,
Makundi 19 ya wakulima eneo la Karas kaunti ya Pokot magharibi yamenufaika na shilingi milioni 19 kutoka kwa serikali ya kaunti kama ufadhili wa kuyawezesha kuendeleza shughuli zao za kilimo.


Akizungumza jumatano alipotoa hundi ya fedha hizo kwa makundi hayo, gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin alisema kila kikundi kitapokea shilingi milioni moja ambazo zitasaidia kuimarisha shughuli zao hasa baada ya kupokea mafunzo kutoka kwa wizara ya kilimo.


Aidha Gavana Kachapin alisema hatua ya serikali yake kuimarisha makundi ya wakulima ni moja ya mbinu ya kutekeleza ajenda ya serikali ya Kenya kwanza chini ya utawala wa rais William Ruto ya Bottom up economic model, inayolenga kuwawezesha wakenya wa hali ya chini.


“Tuna makundi 19 hapa karas ambayo yamekuja pamoja kwa ajili ya maendeleo. Tumetoa hundi ya shilingi milioni 19 ambapo kila kundi litapata shilingi milioni 1. Hii ndiyo tunasema bottom up kwa sababu tunataka yule mama ambaye ako chini aje juu,” alisema Gvn. Kachapin.


Wakati uo huo gavana Kachapin aliyataka makundi hayo kusalia imara katika shughuli zao za kilimo akisema ndiyo njia bora ya kuhakikisha chakula cha kutosha nchini, na kubuni nafasi za ajira hasa wakati huu ambapo ajira zimekuwa nadra nchini.


“Nataka kuyahimiza makundi haya kusalia imara kwa sababu hii ndiyo njia pekee ya kuendeleza nchi hii, na kilimo ndicho mwajiri mkuu wa nchi yetu,” alisema.


Gvana Kachapin aliipongeza wizara ya kilimo kwa kufanikisha mafunzo kwa wakulima hao kuhusu mbinu mbali mbali za kuendeleza kilimo hasa cha ufugaji alichosema kitawapelekea faida kubwa.