Raila analipwa na rais kutuharibia sifa; Moroto

Na Benson Aswani,
Wabunge nchini wameendelea kulalamikia kauli ya rais William Ruto na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kwamba wanajihusisha na maswala ya ufisadi katika kuwachunguza maafisa serikalini na hata magavana.


Wa hivi punde kulalamikia kauli hizo ni mbunge wa Kapenguria, kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto, ambaye amemsuta kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kusisitiza kauli hiyo ya rais akisema huenda wakalazimika kufika mbele ya kamati ya bunge kuhusu sheria kuelezea zaidi kuhusiana na kauli hizo kuwahusu wabunge.


Moroto alidai kwamba huenda Raila anatumika na rais William Ruto kutoa kauli kama hizo za kuwadhalilisha wabunge machoni pa wananchi .


“Tulipokuwa kwenye mkutano, Raila ni rafiki yangu ndio lakini aliropokwa sana. Naona huyu mzee ni kama amelewa pesa ambazo anapewa na huyu mwingine. Hata sioni kama ni Raila anazungumza haya maneno, ni huyu mwingine ambaye anamtumia kuropoka hivyo,” alisema Moroto.


Moroto alisema kwamba licha ya sifa yake ya kuchangia mageuzi ya uongozi nchini na kuhakikisha maswala ya demokrasia, akiwa kiongozi ambaye alishinikiza kuwepo serikali za magatuzi, Raila huenda akavuruga sifa zake wakati huu ambapo anakaribia kustaafu kutoka siasani.


“Lakini kile ambacho nitasema ni kwamba, Raila amechangia makubwa sana nchini. Hata maswala ya ugatuzi ni yeye alishinikiza mpaka tukawa nao. Ila sasa huenda akaharibu sifa zake hasa wakati huu ambapo anakaribia kustaafu kisiasa,” alisema.