Poghisio: Kaunti ya Pokot Magharibi inahitaji mabadiliko haraka iwezekanavyo

Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye pia ametangaza nia ya kuwania kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, ameelezea haja ya kuwepo mabadiliko katika kaunti hiyo.


Akizungumza na wanahabari, Poghisio ambaye aliwahi kuhudumu kama kiongozi wa wengi katika bunge la seneti, alitaja ubadhirifu wa mali ya umma, ukabila na migawanyiko ya kisiasa kuwa moja ya maswala ambayo yanasababisha wakazi wa kaunti hiyo kukosa kupata huduma inavyostahili.


Poghisio alisema wakazi wa kaunti hiyo wamekabiliwa na changamoto nyingi chini ya mazingira haya na sasa ni wakati ambapo wanapasa kumpata kiongozi ambaye ataleta mabadiliko, jukumu alilosema yupo katika nafasi bora ya kutekeleza ikizingatiwa nafasi yake kisiasa kaunti hiyo na taifa kwa ujumla.

“Hii kaunti ya Pokot magharibi inahitaji mabadiliko. Nimefanya uchunguzi wangu kubaini ni kwa nini mambo hayaendi jinsi inavyohitajika, na nimeona viwango vya matumizi mabaya ya mali ya umma, migawanyiko ya kisiasa na ukabila na nimefikia hitimisho kwamba wakazi wameteseka ya kutosha,” alisema Poghisio.


Aliongeza kwa kusema, “Mimi nakuja kama mgombea ambaye hana miegemeo ya kundi lolote la kisiasa ili kuhakikisha kwamba kila mkazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi anapata huduma inayostahili kutoka kwa serikali,”
Alisuta mirengo ya kisiasa ambayo imebuniwa katika kaunti hiyo, aliyosema imechangia migawanyiko miongoni mwa wananchi, swala alilosema ataweza kulishughulikia kwa kuhakikisha wakazi wanaishi kwa umoja iwapo atapewa fursa ya kuongoza kaunti hiyo.


“Utasikia katika kaunti hii kwamba mgombea ana kundi linaitwa massage na mwingine ana kundi linaitwa , mambo ambayo hayamsaidii mwananchi kuelewa kile wanachozungumzia, na sasa wanagombana wao kwa wao hali inayoleta migawanyiko miongoni mwa wananchi,” aliongeza.