Poghisio awasuta wanasiasa wanaotumia fedha kutafuta uungwaji mkono kwenye uchaguzi

Na Benson Aswani
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot Magharibi Samwel Poghisio amekemea pakubwa hulka ya viongozi wa kisiasa ambao wanatafuta nafasi za uongozi kwenye uchaguzi kutumia fedha nyingi kuwahonga wananchi ili kupata uungwaji mkono.
Akizungumza na wanahabari, Poghisio ambaye pia ametangaza nia ya kuwania ugavana wa kaunti hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, alisema wengi wa wanasiasa wanaomwaga pesa kwa wapiga kura nyakati za kampeni ni wale ambao wamepora fedha za umma.
Aidha alisema wengi wa wanasiasa wanaotafuta uungwaji mkono kutoka kwa wananchi kwa kuwapa fedha hawana imani kwamba wataungwa mkono kwa uwezo wao wa kuhakikisha huduma bora kwa wananchi na sasa wanaamua kutumia mbinu tofauti kuingia afisini.
“Hii hulka ya wanasiasa kuwahonga wanachi kwa fedha nyingi ili wapate kupigiwa kura inapasa kukoma. Fedha hizi ambazo wanamwaga kwa umma ni za maendeleo ambazo zimeporwa na hawa wanasiasa.
Na mimi naamini kwamba mwanasiasa yeyote anayewahonga wapiga kura ili apate uungwaji mkono hana imani kwa uwezo wake kuwashawishi wapiga kura,” alisema Poghisio.
Poghisio aliwataka wapiga kura kujitenga na wanasiasa wanaowahonga kwa uungaji mkono wao, na badala yake kuangazia sera na uwezo wa mgombea kuimarisha maisha yao.
Alisema wanasiasa wengi wanaotumia fedha nyingi kutafuta uungwaji mkono, huishia kuiba fedha za umma pindi wanapoingia afisini ili kurejesha fedha walizotumia kwenye kampeni, hali ambayo inalemaza maendeleo kwa mwananchi.
“Ninachowahimiza wananchi ni kwamba ni vyema kuwachagua viongozi ambao wana sera za kuwanufaisha, wala si kuwachagua kulingana na fedha ambazo wamepewa, kwa sababu fedha ambazo wanasiasa hawa wanatumia katika kampeni lazima watazirejesha kwa kuiba mali ya umma wanapoingia afisini,” alisema.
