Poghisio awasuta wanaopinga ujenzi wa chuo kikuu cha Kapenguria

Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameunga mkono kuanzishwa kwa chuo kikuu katika kaunti hiyo hatua anayosema itachangia pakubwa maendeleo ya kaunti.


Poghisio ambaye ametangaza nia ya kuwania ugavana wa kaunti hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, aliwasuta baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wanapinga wazo hilo, akiwataja kuwa maadui wa maendeleo ya kaunti hiyo ambayo imesalia nyuma kwa miaka mingi.


Aidha Poghisio alikosoa hulka ambapo kiongozi anayeingia afisini anatelekeza miradi ambayo ilihasisiwa na mtangulizi wake, hali aliyosema imepelekea kaunti ya Pokot magharibi kutonufaika pakubwa na miradi ya maendeleo licha ya kuwepo ugatuzi.


“Inashangaza kuona kwamba kuna mtu anapinga ujenzi wa chuo kikuu katika kaunti hii, eti kwa sababu imeletwa na mtu kutoka upande ambao haungi mkono. Mambo kama haya ndiyo yanafanya kaunti hii kusalia nyuma kimaendeleo,” alisema Poghisio.


Poghisio alisisitiza kwamba kitakapoanzishwa chuo hicho, wakazi wa kaunti hiyo watapata manufaa ya kupata elimu ya juu kwa karibu kando na kuhakikisha kwamba shughuli za kiabiashara zinaimarika.


“Tunahitaji chuo kikuu katika kaunti hii. Chuo hiki kitasaidia pakubwa katika kuimarisha shughuli za kibiashara pamoja na kuleta elimu ya juu karibu na watoto wetu,” alisema.