Poghisio atetea pendekezo la NG-CDF kuondolewa mikononi mwa wabunge

Na Emmanuel Oyasi,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ametetea kauli ya kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kwamba hazina ya NGCDF ipokonywe wabunge na badala yake isimamiwe na magavana.


Akizungumza na kituo hiki Poghisio alisema kwamba kauli ya Raila inatilia tu mkazo uamuzi wa mahakama kwamba mbunge hastahili kupanga bajeti ya serikali, kugawa fedha hizo na wakati uo huo akitekeleza jukumu la kuwa mwangalizi wa matumizi ya fedha zenyewe.

Aidha alisema ni kinaya kwamba, mbunge ambaye ni mwangalizi wa matumizi ya fedha hizo, pia analazimika kukaguliwa jinsi ambavyo ametumia fedha za hazina ya NGCDF.


“Raila anasisitiza tu mambo ambayo mahakama iliamua kwamba, haiwezekani mbunge awe mwenye kupanga bajeti ya serikali, na pia kupanga jinsi ya kugawa fedha, halafu pia awe mwangalizi kwa wale wanaotumia fedha hizo, na kisha mwenyewe tena atumie pesa zenyewe za CDF, halafu pia akaguliwe jinsi ametumia fedha hizo,” alisema Poghisio.


Hata hivyo Poghisio alitofautiana na pendekezo la Raila la kutaka maseneta kupokonywa jukumu la kuwakagua magavana, na badala yake jukumu hilo kuachiwa waakilishi wadi, akisema hatua hiyo itapelekea bunge la seneti kukosa umuhimu nchini.


“Katiba ndiyo inayoipa seneti nguvu za kuwa mwangalizi wa jinsi magavana wanafanya kazi mashinani. Ukiondoa jukumu hilo kwa maseneta, basi bunge la seneti liondolewe kwa sababu halitakuwa na umuhimu wowote nchini,” alisema.