Poghisio ashutumu migawanyiko miongoni mwa viongozi Pokot Magharibi.

Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameelezea haja ya wadau katika kaunti hiyo kuja pamoja na kusemezana ili kupata mwelekeo wa kisiasa ambao utakuwa wenye manufaa kwa wakazi na kaunti kwa ujumla.
Poghisio alisema migawanyiko ambayo inashuhudiwa miongoni mwa viongozi imeinyima kaunti hiyo nafasi za maendeleo.
Seneta huyo wa zamani alielezea kusikitikia hali kwamba kaunti ya Pokot magharib haiwezi kujivunia nafasi yoyote ya uteuzi katika serikali kuu, hali ambayo imepelekea kukosa sauti ya kushinikiza raslimali zaidi kutoka kwa serikali na kusababisha kaunti hiyo kusalia nyuma kimaendeleo.
“Huu ni mwaka wa kaunti hii kujipanga. Ni lazima serikali hii itushughulikie jinsi inavyoshughulikia wengine. Lakini itatushughulikia vipi iwapo sisi wenyewe tunakatana mikono na miguu? Kwa hivyo huu ni mwaka wa kusemezana tuone ni makosa gani tulifanya ndipo hatuonekani katika taifa hili,” alisema Poghisio.
Wakati uo huo Poghisio alitoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo kuwa makini katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao na kufanya maamuzi ambayo yatapekelekea kuchaguliwa viongozi watakaoweka kipau mbele juhudi za kuwaunganisha wananchi.
“Tujipange kwa njia ya kujenga muundo wa siasa ulio bora ili kila mtu ajue kwamba ukimchagua kiongozi, unamchagua kiongozi ambaye kazi yake ni kuwaunganisha wananchi,” alisema.
