Poghisio ahimiza maandalizi ya kutosha kuhusu mvua za El Nino

Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameihimiza serikali ya kaunti kujiandaa vilivyo kwa ajili ya mvua za elnino ambazo zinatarajiwa kuanza mwezi Octoba kulingana na utabiri wa hali ya anga.
Akizungumza na wanahabari Poghisio ambaye pia ametangaza nia ya kuwania kiti cha ugavana katika kaunti hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, alisema inasikitisha kwamba hadi kufikia sasa hamna hatua muhimu ambazo zimepigwa kwenye maandalizi ya mvua hizo.
Alipendekeza kubuniwa kamati ya ufundi ambayo itasaidia pakubwa katika maandalizi ya kukabili athari ambazo zinasababishwa na mvuo hizo ikizingatiwa kaunti hiyo ni moja ya kaunti ambazo zimekuwa zikishuhudia maporomoko ya ardhi wakati wa mvua kubwa.
“Imesemwa sana kwamba kutakuwa na mvua ya El nino, na mimi nataka kuishauri serikali yetu ijiandae. Kwa sababu kufkia sasa sijaona maandalizi muhimu ambayo yamefanywa. Kunapasa kuwe na kamati ya kiufundi ambayo itahakikisha kwamba maandalizi haya yanafanywa kikamilifu,” alisema Poghisio
Wakati uo huo Poghisio aliitaka serikali kuweka mikakati ya kuelimisha wakazi kuhusu mvua hiyo ili wawe na ufahamu katika hatua za kudhibiti athari ambazo zinaweza kushuhudiwa.
“Unajua ni vigumu sana mtu kuamini kwamba kutakuwa na mvua aina hiyo bila kufunzwa maana ya El nino. Ni lazima watu waambiwe katika vyombo vya habari na katika vikao mbali mbali vya umma kwamba kuna athari ambazo hutokana na mvua hii ili wachukue tahadhari,” alisema.
