Poghisio aelezea wasiwasi kuhusu serikali ya muungano

Na Benson Aswani,
Huenda hatua ya serikali ya rais William Ruto kuunda serikali ya muungano na chama cha ODM ikawa na malengo ya kufanikisha maamuzi ya serikali pamoja na kutimiza malengo ya uongozi wa serikali ya rais Ruto.


Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki, aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio alisema hatua ya vyama vya UDA na ODM kuungana, inatoa fursa ya serikali kupata idadi inayostahili katika kupitisha miswada bungeni na kutekeleleza mabadiliko ya baadhi ya vipengee kwenye katiba.


Aidha Poghisio alielezea hofu kwamba huenda hatua ya kuungana vyama hivyo bungeni ikapelekea serikali kutumia vibaya idadi yake bungeni katika kupitisha maswala ambayo yataweza kuwaumiza wananchi kwa manufaa yake.


“Serikali ya William Ruto imeona itakuwa bora kuwa na idadi nzuri katika bunge wakati wataenda kupitisha ripoti ya NADCO. Na pia wanaweza kubadilisha sehemu zingine katika njia ambayo wamepanga serikali, kwa sababu wapo na idadi ambayo inazidi thuluthi mbili,” alisema Poghisio.


Wakati uo huo Poghisio alisema kwamba hatua ya vyama hivi kuungana italeta utata wa kikatiba ikizingatiwa kiongozi wa wengi na yule wa wachache bungeni watakuwa upande mmoja wa bunge, hatua ambayo itatatiza katika uchangiaji wa mijadala bungeni.


“Kuungana kwa vyama hivi viwili kutaleta utata wa kikatiba kwa sababu kwa mara ya kwanza kiongozi wa wengi bungeni na kiongozi wa wachache wameungana na kuwa upande mmoja. Kwa hivyo swali ni je, itakuwaje katika kuchangia mijadala katika bunge,” alisema.