Owalo aongoza ukaguzi wa mradi wa maji wa Muruny Pokot magharibi

Na Benson Aswani,
Mradi wa maji wa Muruny kaunti ya Pokot magharibi utawafaidi zaidi ya watu alfu 350 punde utakapokamilika.


Akizungumza baada ya kuongoza ukaguzi wa mradi huo, naibu mkuu wa wafanyikazi katika afisi ya rais Eliud Owalo, alisema kando na kuhakikisha kwamba wakazi wanapata maji safi, mradi huo pia unalenga kubuni nafasi za ajira kwa wakazi wa maeneo hayo.

“Mradi huu utatoa maji kwa zaidi ya wakazi 350,000 katika kaunti ya Pokot magharibi utakapokamilika, na pia kubuni nafasi za ajira kwa wakazi,” alisema Owalo.


Kando na mradi huo wa maji, Owalo alikagua miradi mingine ambayo inaendelezwa na serikali katika kaunti hiyo ikiwemo ujenzi wa soko la kisasa eneo la Ortum, miradi aliyosema inalenga kubuni mazingira bora ya kina mama kuendeleza shughuli zao za kibiashara.


“Tumezuru miradi mingine ambayo inaendelezwa na serikali katika kaunti hii ya Pokot magharibi ikiwemo soko la kisasa la Ortum, ambalo litabuni mazingira bora kwa kina mama na dada zetu ambao wanaendeleza shughuli za kibiashara,” alisema.


Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya maji na maendeleo kaskazini mwa bonde la ufa John Lonyangapuo aliusifia mradi huo aliosema ni wenye umuhimu mkubwa kwa kaunti hiyo akisifia pia miradi ambayo imetekelezwa na utawala wa rais William Ruto.


“Huu mradi wa wa maji unahitajika sana katika kaunti hii. Hatuna maji katika mji wetu. Na tutashukuru sana iwapo mradi huu utakamilika haraka iwezekanavyo,” alisema Prof. Lonyangapuo.