Ng’eno atimiza ahadi ya kugharamia elimu ya wasanii wawili Pokot Magharibi

Na Benson Aswani,
Hatimaye mbunge wa Emurwa Dikir Johana Ng’eno ametimiza ahadi yake kugharamia elimu ya vijana wawili wasanii katika kaunti ya Pokot magharibi, ambayo alitoa katika hafla ya mwanamuziki mmoja kaunti hiyo iliyoandaliwa katika shule ya msingi ya Makutano kuadhimisha miaka 10 ya usanii.


Ng’eno ambaye alikuwa mmoja wa wageni waalikwa katika hafla hiyo alielezea kuvutiwa na uwezo wa vijana hao kisanii, akiahidi kugharamia elimu yao, hatua ambayo imepongezwa na jamaa za vijana hao ambao walijiunga rasmi na shule moja ya msingi ya bweni kaunti hiyo, wakiongozwa na nyanya yao Rose Ariang’osiwa.


Aidha mlezi wa vijana hao katika safu ya usanii alielezea ujasiri wao katika majukwaa ambali mbali kuwa kichocheo cha wao kufika kiwango ambacho kilimpelekea mbunge huyo kuchukua hatua ya kugharamia elimu yao.


“Tumefurahi sana kwa hatua ambayo mbunge Ng’eno amechukua kwa ajili ya wajukuu wangu. Kumbe watoto wakiongea sana Mungu ana mipango nao. Nashukuru sana kwa Ng’eno pamoja na Pokot Boy,” alisema Ariang’osiwa.


Kwa upande wake Nashon Aperitum maarufu kama Pokot Boy alipongeza hatua hiyo aliyosema ni muhimu zaidi kwake kutokana na hali kwamba vijana hao walisaidika kupitia hafla aliyoandaa, akitoa wito kwa viongozi wengine kaunti hiyo kuiga mfano huo.


“Namshukuru sana mheshimiwa Ng’eno kwa sababu mambo ambayo alisema kimchezo pale shule ya msingi ya Makutano ameweza kuyatimiza. Pia nawauliza viongozi wengine kaunti hii kuiga mfano huo na kuhakikisha kwamba vipaji ambavyo tanavyo kaunti hii vinakuzwa,” alisema Aperitum.