NAIBU GAVANA POKOT MAGHARIBI AANDIKISHA TAARIFA NA IDARA YA DCI KWA MADAI YA UCHOCHEZI

Na Emmanuel oyasi.

Wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wameisuta serikali ya rais William Ruto kwa kile wamedai kuwahangaisha viongozi wa kaunti hiyo.

Hii ni baada ya naibu gavana Robert Komole kuandikisha taarifa katika makao makuu ya idara ya upelelezi DCI mjini Nakuru alhamisi kuhusu swala zima la ukosefu wa usalama kaskazini mwa bonde la ufa.

Wakiongozwa na Peter Lomada, wakazi hao walisema kwamba naibu gavana amekuwa msitari wa mbele katika kueneza ujumbe wa amani kupitia kuandaa mikutano ya amani hasa maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia uvamizi mipakani pa kaunti hiyo.

“Hii ni serikali ambayo tuliichagua sisi lakini sasa imekuwa ikituandama sana. Hakuna kiongozi katika kaunti hii ambaye hajaagizwa kuandikisha taarifa na idara ya DCI. Kitu kinachotushangaza ni kwamba naibu gavana ambaye amekuwa msitari wa mbele katika kuhubiri amani kanda ya kaskazini mwa bonde la ufa sasa anakamatwa kwa maswala yasiyoeleweka.” Walisema.

Aidha wakazi hao walishutumu kile walidai kukiukwa haki za naibu gavana kwa  kuhangaishwa na maafisa hao katika mchakato mzima wa kuchukua taarifa yake kabla ya kuachiliwa baadaye alhamisi, wakimtaka rais William Ruto kuingilia kati na kusuluhisha swala la mipaka wanalosema ndio chanzo cha swala zima la utovu wa usalama.

“Naibu gavana ana haki kama wakenya wengine. Haki zake zinapaswa kuheshimiwa. Hii hatua ya maafisa wa DCI kumhangaisha naibu gavana wetu na kumnyima haki ni mbaya sana. Tunaomba rais atafute suluhu kwa tatizo la mipaka ya kaunti ya Pokot na Turkana kwa sababu hiki ndicho chanzo cha utovu wa usalama.” Walisema.

Akizungumza muda mfupi tu baada ya kuachiliwa huru Bw. Komole alisema kwamba hahusiki katika njia yoyote na madai ya uchochezi ambayo yameibuliwa dhidi yake akisema kwamba viongozi wa kaunti hiyo wanahangaishwa kwa sababu zisizo na msingi.

Haya madai ya uchochezi ambayo nashutumiwa nayo hata mimi siyafahamu. Kwa sababu nimekuwa nikizunguka kaunti ya Pokot magharibi hadi Uganda nikihubiri amani kwa watu wetu. Sijafurahia hii tabia ya kuwahangaisha viongozi wa kaunti ya Pokot magharibi.” Alisema Bw. Komole.