Murkomen atoa hakikisho la kukabili ‘wala watu’ Pokot magharibi

Na Benson Aswani,
Waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Kipchumba Murkomen amewahakikishia wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kwamba serikali itakabiliana kikamilifu na swala la watoto kutekwa nyara na kupatikana wameuliwa huku baadhi ya viungo vikinyofolewa kwenye miili yao, katika visa ambavyo vimekuwa vikiripotiwa hasa eneo la Bendera kaunti hiyo.
Murkomen alisema kwamba kando na kuwahakikishia waathiriwa wa visa hivyo haki, serikali itahakikisha kwamba idara ya usalama inapata imani ya wananchi katika juhudi zake za kuhakikisha usalama wa wananchi.
Murkomen ambaye alikuwa akizungumza na wanahabari katika afisi za kamishina wa kaunti hiyo mjini Kapenguria alisema kwamba ni jukumu la serikali kuhakikisha usalama wa watoto kila sehemu walipo na hata wananchi kwa ujumla wanapoendeleza shughuli zao za kila siku.
“Hili ni swala ambalo tunawahakikishia wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kwamba tunaenda kukabiliana nalo kikamilifu ili waathiriwa wapate haki. Lakini si kuhakikisha tu haki kwa waathiriwa, bali pia usalama wa wakazi wote kwa ujumla,” alisema Murkomen.
Murkomen alihusisha visa hivyo na hali kwamba kaunti hiyo ipo eneo la mipakani ambapo raia kutoka mataifa ya kigeni wanaingia bila ya idhini, na pia kutumika kama eneo la kuendeleza biashara ya binadam, akisema serikali inaweka mikakati thabiti ya kukabili hali hiyo.
“Hii ni kaunti ambayo ipo mipakani na hali hii inachangia idadi kubwa ya raia kutoka mataifa mengine kuingia kinyume cha sheria, hali ambayo imechangia kukithiri visa kama hivi. Kwa hivyo kama serikali tunaweka mikakati ya kuzuia hali hii,” alisema.
Ziara hiyo ya waziri Murkomen kaunti ya Pokot magharibi ilipongezwa na viongozi kaunti hiyo waliyosema ilikuwa na manufaa makubwa.
Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong alisema limekuwa tamanio la viongozi kaunti hiyo kwa waziri huyo kuja kusikiliza kutoka kwa viongozi mashinani kuhusu jinsi ya kushughulikia swala zima la usalama.
Aidha Lochakapong alisema ujio wa waziri huyo uliwezesha viongozi wote kaunti hiyo kuja pamoja na kujadili maswala ya kaunti na jinsi ya kuimarisha huduma kwa wananchi, swala ambalo limekuwa nadra kufanyika kutokana na tofauti za kisiasa.
“Waziri amefanya jambo la muhimu kuja kuzungumza na wakazi wa kaunti hii. Na kama viongozi tunamshukuru kwa hilo. Pia amehakikisha kwamba viongozi wote wamekuja pamoja na kuangazia maswala muhimu ya wananchi, swala ambalo limekuwa vigumu sana kufanyika,” alisema Lochakapong.
Lochakapong alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa maafisa wenye jukumu la kuhakikisha usalama kwa wananchi kutekeleza shughuli zao kulingana na sheria bila ya kushinikizwa, kuhitilafiwa au kugemea upande wowote.