Msako dhidi ya pombe haramu waendelezwa eneo bunge la Kapenguria

Na Benson Aswani,
Idara ya polisi eneo bunge la Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na machifu wanaedeleza msako dhidi ya ugemaji wa pombe haramu katika juhudi za kukabili biashara hiyo ambayo imeharamishwa nchini.
Kamanda wa polisi eneo bunge la Kapenguria Patrick Nyanga alisema kwamba oparesheni hiyo inalenga zaidi wagemaji na wasambazaji wa pombe hiyo, ikiwa tayari lita alfu 3,390 za pombe aina ya kangara zimeharibiwa na lita 160 za pombe aina ya chang’aa kutoka kwa mgemaji sugu eneo la Kamarkech zikinaswa.
“Ni vita tulianza kuhakikisha kwamba hakuna pombe haramu eneo bunge la Kapenguria. Tunalenga zaidi wagemaji na wasambazaji katika zoezi hili, ili kuhakikisha tunamaliza chanzo ndio tuweze kukabili wale ambao wanatumia pombe hiyo,” alisema Nyanga.
Ni kauli iliyosisitizwa na chifu wa kata ya Kapenguria Bi. Dorcas Aleutum ambaye alisema vijana wengi wamepoteza maisha kwa kubugia pombe hiyo haramu na wengine kuacha masomo, akiwataka wakazi kujitenga na biashara hiyo.
“Wengi wa vijana eneo hili wamepoteza maisha kufuatia unywaji wa pombe haramu. Tunaomba jamii kujitenga na biashara hii kwa sababu hata vitu wanavyotumia kutengeneza ni hatari kwa afya ya binadamu,” alisema Bi. Aleutum.
Wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakilalamikia madhara ambayo yamesababishwa na biashara hiyo ya ugemaji wa pombe haramu, ikiwemo kuathiri afya ya watumiaji na kuchangia utovu wa usalama.
Walipongeza oparesheni hiyo ambayo walielezea imani kwamba itasaidia kukabili visa hivyo.