Mpango wa ‘Ondoa Nyasi’ pokot magharibi washika kasi

Na Benson Aswani,
Mpango unaondelezwa na gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin kuwajengea wakazi nyumba za mabati maarufu ondoa nyasi ni wenye manufaa makubwa hasa ikizingatiwa nyasi ambazo zinatumika na wakazi wengi maeneo ya mashinani zimekuwa nadra kupatikana wakati huu.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo katika shule ya upili ya Kacheliba, mwakilishi wadi ya Kodich Paul Loktari aidha alisema kadri siku zinapozidi kusonga, bajeti ya mpango huo itaongezwa ikizingatiwa idadi kubwa ya wanaohitaji kunufaika.

“Hapa kodich hakuna nyasi. Sasa wakazi wanalazimika kwenda Uganda kutafuta nyasi na hata nyasi zenyewe hazikai kwa muda. Kwa hivyo mpango huu wa gavana utawafaa sana wakazi wa eneo hili,” alisema Loktari.


Kauli yake ilisisitizwa na wakazi wa eneo hilo la Kacheliba wakiongozwa na Michael Siyakin ambao walisema kwamba eneo hilo limesalia nyuma pakubwa kimaendeleo, na kwamba hatua hiyo itawapunguzia pakubwa changamoto wanazopitia kuishi katika nyumba zilizoezekwa kwa nyasi.


“Tunafurahia mikakati ya kaunti kutuletea mabati, kwa sababu sisi eneo hili tupo nyuma sana kimaendeleo, na tunapitia changamoto nyingi sana kuishi katika nyumba hizi za nyasi,” alisema Siyakin.


Uongozi wa shule ya upili ya Kacheliba chini ya mwalimu mkuu Dina Lonyangapoi, ulielezea kunufaika pakubwa kupitia mpango huo kando na miradi mingi ambayo inasubiriwa kutekelezwa kwa ufadhili wa serikali ya kaunti.


“Hii shule ni ya kitambo sana na mabati yamezeeka. Kwa hivyo kama shule tulianzisha mpango wa kuboresha madarasa yetu. Na kwa kuwa mpango huu wa ondoa nyasi umezinduliwa hapa, sisi kama shule pia tumenufaika pakubwa,” alisema Bi. Lonyangapoi.