Mhudumu wa afya amlawiti mgonjwa Murpus

Na Benson Aswani,
Mhudumu mmoja wa afya mwenye umri wa miaka 55 eneo la Murpus kaunti ya Pokot magharibi anazuiliwa na maafisa wa polisi kwa madai ya kumlawiti kijana mmoja, mwanafunzi wa gredi ya nane mwenye umri wa miaka 15 ambaye alifika katika zahanati ya Murpus kupokea matibabu.


Akilaani vikali kisa hicho mwenyekiti wa mtandao wa Child Protection Network Carolyne Menach, alidai mwathiriwa alifika katika zahanati hiyo kutafuta matibabu kabla ya mhudumu huyo kumshawishi na kumwelekeza chumbani, ambapo alimtendea unyama huo.


Alisema kwa sasa kijana huyo ambaye ni mwanafunzi wa gredi ya nane anaendelea kupokea matibabu hospitalini.


“Tuna mhudumu mmoja wa afya wa nyanjani CHP ambaye amemlawiti mwanafunzi wa gredi ya nane ambaye alikuwa amekwenda kutafuta matibabu katika zahanati ya Murpus. Nakemea sana kitendo hicho na naomba hatua kali zichukuliwe dhidi yake,” alisema Menach


Ni kisa ambacho kilithibitishwa na mzee wa mtaa eneo hilo Josephat Adumonyang ambaye alitaka mhudumu huyo kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwani huenda si mara ya kwanza kutekeleza uovu huo.


“Hicho kitendo ni cha aibu sana na mhudumu huyo hafai kuruhusiwa kurejea huku kwa sababu hatumtaki tena. Mtu ambaye tulimwamini kwamba watu wetu wako salama kwake kumbe anawatendea uovu kama huu,” alisema Adumonyang