Mashirika ya jamii yapongezwa kwa kuchangia kupungua ukeketaji pokot magharibi

Na Emmanuel Oyasi,
Msaidizi wa kamishina eneo la Chesogon kaunti ya Pokot magharibi Peter Njuguna amepongeza mikakati ambayo imewekwa na serikali kwa ushirikiano na mashirika mbali mbali ya kijamii ambayo imepelekea kupungua pakubwa visa vya ukeketaji eneo hilo.


Akizungumza katika hafla moja eneo la Chepkokou, Njuguna alisema uhamasisho ambao unaendelezwa na baadhi ya mashirika ya kijamii kaunti hiyo kwa ushirikiano na wadau wengine umesaidia katika kupunguza pakubwa visa hivyo, ambapo wengi wa wakazi sasa wanafahamu madhara ya tamaduni hiyo.


Aidha Njuguna aliendelea kuwahimiza wakazi kujitenga na tamaduni hiyo aliyosema kando na kuharamishwa na serikali, inasababisha wengi wa watoto wa kike kukosa kuafikia ndoto zao maishani kwani wengi wao huolewa pindi wanapokeketwa.


“Kwa muda ambao nimekaa hapa nawezasema ukeketaji umerudi chini. Haya mashirika ya kijamii pamoja na wadau wengine yametusaidia pakubwa katika kuhamasisha jamii dhidi ya visa hivi na sasa wanafahamu madhara yake,” alisema Njuguna.


Kauli yake ilisisitizwa na chifu wa Chepkokou Joseph Kasirtich ambaye aidha alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa vijana ambao walikamilisha masomo yao ya shule za upili kujiunga na vyuo vya kiufundi ili kupata ujuzi utakaowafaa katika kujikumu kimaisha.


“Hapa kwetu kuna vijana wengi sana ambao walimaliza shule za upili na hawana cha kufanya. Nawahimiza kujiunga na vyuo vya kiufundi, kupata ujuzi ambao utawasaidia kujikimu kimaisha,” alisema Kasirtich.