Makamanda wa kaunti tano za bonde la ufa wakutana kuweka mikakati ya kukabiliana na mihadarati

Na Emmanuel Oyasi,
Kamanda wa polisi kanda ya bonde la ufa Samwel Ndanyi Jumatano, Januari 14, 2026 aliongoza kikao cha usalama kinachohusisha makamanda wa polisi kaunti tano za bonde la ufa kwenye ukumbi wa mtelo mjini Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi.


Akizungumza na wanahabari baada ya kikao hicho, Ndanyi alisema kilihusu kuweka mikakati ya jinsi ya kukabili biashara ya mihadarati katika kaunti hizo ambazo alisema zipo mipakani swala linalochangia kuingizwa mihadarati kwa urahisi kutoka mataifa mengine.

Aidha alisema wanalenga kuweka mkakati wa kuhakikisha kuna mawasiliano bora kati ya wakuu wa usalama kutoka katika kaunti za bonde la ufa ili kuimarisha vita dhidi ya dawa za kulevya na pombe haramu.


“Tumeona tuje tukutane hapa kama makamanda wa kaunti tano la bonde la ufa kupanga jinsi ya kukabiliana na mihadarati. Mnavyoelewa ukanda huu unapakana na mataifa kama vile Ethiopia na Sudan na tunashuku kwamba kuna vitu kadhaa ambavyo vinaweza kuwa vinatoka katika mataifa jirani,” alisema Ndanyi.


Wakati uo huo Ndanyi alisema idara ya usalama itashirikiana na wadau mbali mbali ikiwemo shirika la kukadiria ubora wa bidhaa nchini KEBS miongoni mwa wadau wengine katika vita hivi ili kuhakikisha kwamba vinafaulu.


“Kile tunachosisitiza sana ni kufanya kazi na vitengo vingine kama vile KEBS, NACADA, KRA. Utakuta kwamba mwelekeo ambao tulikuwa tumechukua awali tulikuwa tunajikuta peke yetu ambapo ilikuwa vigumu kukabiliana na swala hili,” alisema.