Maafisa wa kliniki Pokot magharibi wagoma

Na Benson Aswani,
Maafisa wa kiliniki katika kaunti ya Pokot magharibi wameungana na wenzao kote nchini kwa mgomo unaolenga kushinikiza serikali za kaunti kutelekeza mkataba wao wa maelewano CBA.


Akizungumza baada ya kukutana na maafisa hao, mwakilishi wa muungano wa maafisa wa kliniki KUCO eneo la kaskazini mwa bonde la ufa na magharibi ya nchi Xevia Wafula aliusuta uongozi wa kaunti hiyo kwa kile alisema kuwahadaa maafisa hao kwa muda sasa kuhusu kutekelezwa mkataba huo.


“Maafisa wa kliniki katika kaunti hii waliahidiwa na gavana kwamba atawashughulikia matakwa yao, lakini sasa umesalia uongo hadi kufikia sasa. Kaunti zote nchini zimetia saini mkataba wa maelewano CBA ila maafisa hao katika kaunti hii hawajaona chochote,” alisema Wafula.

Kulingana na mwenyekiti wa maafisa hao katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi Michael Lotekori, tangu mwaka 2017 serikali ya kaunti haijaonyesha nia ya kusaini mkataba wa kurejea kazini na maafisa hao, hatua ambayo imewanyima nyongeza ya mishahara na marupurupu.


“Tangu mwaka 2017 kaunti hii haijasaini mkataba wa CBA na mpango wa kurejea kazini. Hali hii imechelewesha sana nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa kliniki,’ alisema Lotekori.


Kando na mishahara, wahudumu hao wanalalamikia kutopandishwa vyeo wakitaka pia maafisa ambao wanahudumu kwa kandarasi ya muda kuajiriwa rasmi, wakiapa kuendelea na mgomo wao hadi matakwa yao yatakapotekelezwa.